GENERAL NEWS

“Aliniahidi Helikopta”: Mashahidi Wafichua Mambo Mapya Katika Kesi ya Pastor Mackenzie

Alisema mwanawe mkubwa, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kibabii, alimuambia Mackenzie ni “mtumishi wa kweli wa Mungu” na akamshawishi wauze mali zao zote na kuhamia Shakahola wakiamini watakuwa matajiri

Mashahidi wameendelea kufichua siri mpya katika Mahakama Kuu ya Mombasa kuhusu kesi ya mauaji inayomkabili mchungaji Paul Mackenzie na washirika wake 30, wakisimulia jinsi ndugu na jamaa zao walivyodanganywa kujiunga na mafundisho yenye utata ya dhehebu la Good News International Church huko Shakahola

Benson Mutimba, mkazi wa Webuye, aliiambia mahakama kuwa Mackenzie alimwahidi kumununulia helikopta iwapo angeendelea kuwa mwaminifu kwa mafundisho yake. Mutimba, ambaye alikuwa shahidi wa 57 wa upande wa mashtaka, alisema watoto wake wawili wenye umri wa miaka 27 na 16 waliacha shule baada ya kufundishwa kwamba elimu ni dhambi

Alisema mwanawe mkubwa, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kibabii, alimuambia Mackenzie ni “mtumishi wa kweli wa Mungu” na akamshawishi wauze mali zao zote na kuhamia Shakahola wakiamini watakuwa matajiri

“Aliniambia Mackenzie alikuwa ameahidi kumpa helikopta kama angeendelea kufuata mafundisho yake,” Mutimba alieleza mahakamani

Baada ya watoto wake kutoweka, aliripoti kwa DCI, ambao walipata simu yao moja ikiwa imefuatiliwa hadi Malindi, karibu na kituo cha Mackenzie. Kumbukumbu za Safaricom zilionyesha mwanawe alituma KSh 200 kwa nambari ya Mackenzie alipowasili Ukunda, Kaunti ya Mombasa

Jesca Safari Kone, shahidi wa 58, alisema alipoteza mawasiliano na dada zake watatu waliokwenda Shakahola, na baadaye alijua wote pamoja na watoto wao watano walifariki msituni humo

Esther Anyango, shahidi wa 59, alisema binti yake alihamia Shakahola na mumewe kutoka Likoni, na baadaye akaambiwa binti yake alifariki wakati wa kujifungua. Hadi sasa, hajajua alipo mkwewe na wajukuu wawili waliopotea

 Pia soma  : Mazungumzo ya Makubaliano Kati ya Obado na EACC Yavunjika

Roseline Anivisa Asena, shahidi wa 60 kutoka Embakasi South, alisema kaka yake alianza kufuata mafundisho ya Mackenzie kwa bidii, akawatoa watoto wake shuleni na kukataa matibabu

“Aliteketeza ripoti za shule na vyeti vya kuzaliwa vya watoto wake,” alisema. Baadaye alimwona kaka yake kwenye runinga akiwa Shakahola, na mkewe akionekana amedhoofika sana baada ya kuokolewa

Watoto waliopatikana na kuwekwa Mayungu Children’s Home waliambia Roseline kuwa watoto watatu wa kaka yake walifariki na kuzikwa Chakama, huku mmoja akifariki usiku na mwingine akipatikana akiwa hawezi kuzungumza wala kutembea

Florence Mwahita Mwaigo, shahidi wa 61, alisema mwanawe Alfonce Chomba, mmoja wa washitakiwa, alipoteza mkewe Gloria Riziki na mtoto wao Nathan Chomba huko Shakahola. Alisema mwanawe alikuwa mfuasi sugu wa Mackenzie, aliyekataa elimu na tiba akiamini ni dhambi

Upande wa mashtaka unaendelea kujenga ushahidi wake dhidi ya Mackenzie na wenzake wanaokabiliwa na mashtaka kuhusiana na vifo vya watu 191 waliopatikana msitu wa Shakahola

Mwandishi : Mweru Mbugua

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button