courts

Mazungumzo ya Makubaliano Kati ya Obado na EACC Yavunjika

EACC iliambia mahakama kwamba ingawa kikao kilifanyika Oktoba 30 katika ofisi za DPP kama ilivyoelekezwa awali, mazungumzo hayo yaligonga mwamba baada ya pande husika kutofautiana katika tafsiri ya maagizo ya awali ya mahakama

Mazungumzo ya makubaliano ya kutafuta suluhu (plea bargain) kati ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuhusu kesi ya ufisadi inayomkabili aliyekuwa Gavana wa Migori, Okoth Obado, yamevunjika, na kuilazimu mahakama kuingilia kati kusikiliza ombi hilo

Mahakama ya Ufisadi ilifahamishwa kuwa taasisi hizo mbili zilishindwa kufikia makubaliano kuhusu masharti ya makubaliano hayo yaliyopendekezwa katika kesi inayoendelea dhidi ya Obado

EACC iliambia mahakama kwamba ingawa kikao kilifanyika Oktoba 30 katika ofisi za DPP kama ilivyoelekezwa awali, mazungumzo hayo yaligonga mwamba baada ya pande husika kutofautiana katika tafsiri ya maagizo ya awali ya mahakama

“Tuliwasilisha wasiwasi wetu kuhusu makubaliano hayo mbele ya mahakama hii. Tulikubaliana kuendelea na mazungumzo zaidi ili kuhakikisha makubaliano yanaandikwa kwa mujibu wa sheria, lakini kwa bahati mbaya, mazungumzo hayo yalivunjika,” afisa wa EACC aliambia mahakama

Tume hiyo sasa imeomba mahakama iamue kama makubaliano yaliyowasilishwa na DPP yanakidhi matakwa ya kisheria

Mawakili wa utetezi waliunga mkono msimamo wa EACC, wakithibitisha kuwa kikao kilifanyika lakini hakikufikia mwafaka wowote

“Mimi ninathibitisha tulikutana katika ofisi ya DPP tarehe 30 na ninaunga mkono msimamo uliowasilishwa na Nora. Tunaomba mahakama itoe uamuzi kuhusu jinsi pande zinavyopaswa kuendelea,” wakili wa utetezi alisema

 Pia soma : Wafu Wawili Wauawa Kwenye Ghasia za Kisiasa Kabla ya Uchaguzi Mdogo wa Kasipul

Wakili mwingine wa upande wa watuhumiwa aliongeza kuwa mvutano huo umetokana na “tafsiri tofauti” za sheria zinazosimamia makubaliano ya aina hiyo

Mahakama imepanga kusikiliza kesi hiyo tena tarehe 8 Desemba ili kuamua mwelekeo wa maombi hayo ya makubaliano ya kutafuta suluhu

Mwandishi : Mweru Mbugua

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button