POLITICS

EACC Yashtaki Gavana Wamatangi na Wengine 13 kwa Ufisadi wa Zabuni wa KSh.813 Milioni

Kulingana na uchunguzi wa EACC, Wamatangi alishirikiana na kampuni hizo kuwasilisha nyaraka bandia na kutoa taarifa za uongo kuhusu uwezo wao wa kiufundi ili kushinda zabuni hizo “kwa hasara ya umma"

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imewasilisha kesi kortini ikitaka kurejesha zaidi ya shilingi milioni 813 kutoka kwa Gavana wa Kiambu, Kimani Wamatangi, na washukiwa wengine 13 kwa madai ya kuhusika katika ufisadi wa zabuni za ujenzi wa barabara

Kwa mujibu wa hati za mahakama zilizowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Nairobi, EACC inadai kuwa Wamatangi alitumia wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Barabara, Uchukuzi na Makazi kuingilia mchakato wa utoaji wa zabuni kwa kampuni zinazohusishwa naye binafsi

Madai hayo yanahusiana na mikataba ya ujenzi iliyotolewa kati ya mwaka wa kifedha 2018/2019 na 2021/2022 na mamlaka tatu za barabara nchini Kenya National Highways Authority (KeNHA), Kenya Urban Roads Authority (KURA) na Kenya Rural Roads Authority (KeRRA)

Kulingana na uchunguzi wa EACC, Wamatangi alishirikiana na kampuni hizo kuwasilisha nyaraka bandia na kutoa taarifa za uongo kuhusu uwezo wao wa kiufundi ili kushinda zabuni hizo “kwa hasara ya umma”

“Tuhuma zinaonyesha kwamba mshtakiwa wa kwanza alitumia mamlaka yake vibaya ili kujipatia manufaa binafsi pamoja na washitakiwa wenzake,” EACC ilieleza katika hati ya kesi

EACC imeongeza kuwa Wamatangi alijaribu kuficha umiliki wake katika kampuni hizo kwa kuhamisha uongozi kwa jamaa zake wa karibu na watu wa kujitokeza kama wawakilishi, huku akiendelea kuwa msaini wa akaunti za kampuni hizo na kufanya miamala kupitia kwake

Kampuni tano zimeorodheshwa kuwa zilipokea malipo yasiyo halali kutoka KeNHA, KURA na KeRRA. Kampuni hizo ni Quick Fix Auto Garage Ltd, King Realtors Co. Ltd, King Group Co. Ltd, King Construction Co. Ltd, na Lub Plus Oil & Energy Co. Ltd

  Pia soma : Mazungumzo ya Makubaliano Kati ya Obado na EACC Yavunjika

Kwa jumla, kampuni hizo zilikusanya KSh.726 milioni kutoka KeNHA na KURA, na KSh.86 milioni kutoka KeRRA, zikiwa na jumla ya KSh.813,145,532.40 ambazo EACC inadai ni mapato ya ufisadi

Tume hiyo sasa inataka mahakama kutoa amri za kuhifadhi mali za washitakiwa hadi kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa

Jaji Lucy Njuguna mnamo Novemba 5, 2025, aliruhusu EACC kuwatumia hati za mashtaka washitakiwa, huku ombi la zuio likipangiwa kusikilizwa tarehe 18 Novemba 2025

Mwandishi : Mweru Mbugua

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button